Hebrews 10

Dhabihu Ya Al-Masihi Ni Mara Moja Tu

1 aTorati ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu. 2 bKama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi. 3 cLakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka, 4 dkwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

5 eKwa hiyo, Al-Masihi alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka,
bali mwili uliniandalia;

6 sadaka za kuteketezwa na za dhambi
hukupendezwa nazo.

7 fNdipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja,
imeandikwa kunihusu katika kitabu:
Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ”

8 gKwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe). 9 hKisha akasema “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili. 10 iKatika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Isa Al-Masihi alioutoa mara moja tu.

11 jKila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. 12 kLakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. 13 lTangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, 14 mkwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

15 nPia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:
16 o“Hili ndilo Agano nitakalofanya nao
baada ya siku hizo, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,
na kuziandika katika nia zao.”

17 pKisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao
sitakumbuka tena.”

18Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.

Wito Wa Kuvumilia

19 qKwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Isa, 20 rkwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake, 21 sbasi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22 tsisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Al-Masihi na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 uTushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24 vTuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 wWala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

26 xKama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 yLakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 zYeyote aliyeikataa sheria ya Musa alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 aaJe, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 abKwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 acNi jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

32 adKumbukeni siku zile za kwanza, ambazo mkiisha kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu. 33Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliofanyiwa hivyo. 34 aeMliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

35 afKwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno. 36 agInawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi. 37 ahKwa kuwa bado kitambo kidogo tu, “Yeye ajaye atakuja wala hatakawia.

38 aiLakini mwenye haki wangu
ataishi kwa imani.
Naye kama akisitasita,
sina furaha naye.”

39 ajLakini sisi hatumo miongoni mwa hao wanaositasita na kuangamia, bali tuko miongoni mwa hao wenye imani na hivyo tunaokolewa.
Copyright information for SwhKC